Dalili Na Madhara Ya Kisukari

 

madhara ya kisukari

 

Tuliona katika ukurasa mwingine kuwa kisukari ni ugonjwa ambao humsababishia mtu kuwa na kiwango kikubwa cha sukari katika damu na kushindwa kuitumia sukari hiyo ipasavyo ili kumpa nguvu na hivyo sukari hiyo kutoka nje ya mwili wa mgonjwa kupitia njia ya mkojo. Ugonjwa huu pia huitwa Diabetes Mellitus, maneno yanayotokana na kigiriki na kilatini. Diabetes linatokana na kigiriki likimaanisha kijibomba kinachonyonya maji na mellitus linatokana na neno la kilatini “Mel” lenye maana ya asali, hivyo diabetes mellitus ni “kunyonya maji yenye utamu kama asali” baada ya madaktari wa enzi hizo kugundua kuwa mkojo na damu ya mgonjwa wa kisukari vilikuwa na glucose kwa wingi sana.

Wachina wa zamani nao waligundua kuwa mchwa walijaa kwa kwingi kwenye eneo la mkojo wa mtu mwenye kisukari kutokana na mkojo huo kuwa mtamu na wakatoa neno “Sweet Urine Disease” -Ugonjwa wa kutoa mkojo mtamu.

 

Insulin Na Kongosho

 

Insulin ni homoni inayotoa ishara kwa seli za mwili ili ziweze kuchukua glucose kotoka kwenye damu na kuitumia katika kuupa mwili nguvu na kuujenga. Kama kiwango cha insulin mwilini ni kidogo au hakuna insulin kabisa katika mwili, glucose haitachukuliwa na seli za mwili hivyo kusababisha mwili kuyeyusha mafuta yaliyomo mwilini ili upate nguvu.

Insulin karibu za wanyama wote hufanana, tofauti ni katika nguvu ya ufanyaji wake wa kazi. Kwa mfano, insulin ya nguruwe “Porcine insulin”, inafanana sana na insulin ya binadamu, hii ikiwa na maana kuwa binadamu anaweza kutumia insulin ya wanyama. Lakini kwa bahati nzuri, insulin inaweza kutengenezwa kwenye maabara.

Kongosho ni sehemu ya viungo vilivyo katika mfumo wa uyeyushaji (mmeng’enyo) wa chakula na kinapatikana sehemu ambapo mbavu hukutana kwa chini. Kongosho lina umbo la jani na lina urefu upatao kama nchi sita. Kongosho ina kazi ya kutengenza insulin na homoni zingine za kusaidia uyeyushaji wa chakula.

 

Dalili Za Kisukari Ni Zipi?

 

Baada ya kujikumbusha hayo, sasa tutazame mambo ambayo yakikutokea ujue kwamba ni dalili za kuwa na ugonjwa huu wa kisukari. Watu wengi wanakuwa na ugonjwa huu bila kujijua kwa sababu dalili za awali za ugonjwa huu hazimsababishii mtu kushindwa kuendelea na shughuli zake za kawaida, lakini ni vizuri kuugundua ugonjwa huu katika hatua zake za awali ili kuepukana na madhara makubwa yanayoweza kutokea baadaye. Tutaorodhesha hapa dalili zinazojionyesha mara nyingi zaidi:

Kukojoa mara kwa mara: Jee, umekuwa na tabia ya kwenda kupata haja ndogo mara kwa mara? Kama jibu ni ndiyo, basi figo zako sasa haziwezi kuirudisha glucose kwenye mfumo wa damu na badala yake zinachukua maji kutoka kwenye damu na kusababisha kibofu kijae mara kwa mara.

Kiu Isiyoisha: Kama unakojoa mara kwa mara, utapata kiu isoisha kwa sababu mwili unahitaji kurudisha maji uliyopoteza kwenye mkojo.

Njaa Kali: Kama isulin yako haifanyi kazi au kama huna insulin, mwili wako unakosa glucose ya kuupa nguvu. Katika kutafuta njia nyingine ya kupata nguvu, mwili utakuwa na njaa ili uupatie chakula.

Kuongezeka kwa uzito (unene): Hii inatokana na dalili ya kusikia njaa kali.

Kupungua uzito kusiko kawaida: Hili huwatokea zaidi wagonjwa wa Type 1 Diabetes kwa sababu kwa kukosa insulin na seli kukosa chanzo cha kupata nguvu, mwili huanza kuvunjavunja misuli na kuyeyusha mafuta ya mwili ili upate nguvu hiyo hali inayochangiwa zaidi na tabia ya kisukari cha aina hiyo kujitokeza kwa ghafla.

Uchovu wa mwili: Mwili unapokosa glucose ya kuzipa seli nguvu, uchovu hutokea.

 

dalili za kisukari

 

Hasira: Hasira zinaweza kuwa ni sababu ya mwili kukosa nguvu.

Kutoona vizuri: Ugonjwa huu husababisha mtu kushindwa kuviona vitu vizuri. Tatizo hili hutibika lakini mara nyingine hali huweza kuwa mbaya kiasi cha kuwa na tatizo la kudumu au kupata upofu.

Vidonda kutopona vizuri au haraka: Unapokuwa na sukari nyingi katika damu, uwezo wa mwili kuponya vidonda hupungua.

Magonjwa ya ngozi: Mwili wenye sukari nyingi ndani ya damu huwa na uwezo mdogo sana wa kujiponya kutokana na maambukizi ya wadudu. Wanawake wenye kisukari huwa na maambukizi zaidi na hupata shida kubwa ya kuponya maambukizi ya sehemu nyeti za miili yao.

Kuwashwa kwa ngozi: Kuwashwa kwa ngozi mara nyingine ni dfalili ya kuwa na kisukari.

Kuwa na fizi nyekundu au zilizovimba: Fizi nyekundu na/au zilizovimba huweza kuwa kuwa ni dalili ya kuwa na ugonjwa wa kisukari, mara nyingine meno hulegea.

Uwezo mdogo wa kushiriki tendo la ndoa: Hili ni tatizo hasa la wanaume wenye umri unaozidi miaka 50, ambapo mara nyingi watakosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu au uwezo wao wa kufanya tendo hilo kufa kabisa (Erectile Dysfunction).

Ganzi mikononi au miguuni: Uzidifu wa sukari mwilini huweza kuharibu neva au mishipa midogo ya damu inayolisha neva, hivyo kusababisha hali ya ganzi mikononi au miguuni.

 

 

madhara ya kisukari

 

Madhara Ya Kisukari

 

Kama ugonjwa wa kisukari hautadhibitiwa ipasavyo, madhara makubwa huweza kutokea. Baadhi ya madhara ambayo yamehusishwa na ugonjwa huu ni kama ifuatavyo:

  • Matatizo ya macho-glucoma, cataracts na mengineyo.
  • Matatizo ya miguu-vidonda na gangrene ambavyo mara nyingine husababishwa miguu ikatwe.
  • Matatizo ya moyo-pamoja na upungufu wa damu inayoelekea kwenye misuli ya moyo.
  • Hypertension-ambayo huweza kulsababisha figo kushindwa kufanya kazi, matatizo ya macho, magonjwa ya moyo na kiharusi.
  • Matatizo ya kusikia-kisukari husababisho tatizo la kushindwa kusikia vizuri.
  • Gastroparesis-misuli ya tumbo kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
  • Kiharusi (Stroke)-endapo blood pressure, cholesterol na sukari havitadhibitiwa, uwezekano wa kupatwa na kiharusi huwa ni mkubwa sana.
  • Ugumba-kisukari humfanya mgonjwa ashindwe kufanya tendo la ndoa.

Katika ukurasa unaofuta tutajadili chakula na mazoezi ya mgonjwa wa kisukari na ukurasa mwingine wa mbele utajadili tiba ya kisukari kwa kutumia insulin.

Usisite kuuliza swali au kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo, tutafurahi sana kukujibu.

Pata ushauri zaidi kwa kututumia ujumbe kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au tutumie barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Ukurasa  1    2    3     4

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii

404 Not Found

404 Not Found


nginx/1.10.3