KUSHINDWA KUFANYA TENDO LA NDOA KUTOKANA NA WASIWASI

 

 

kushindwa kufanya tendo la ndoa

 

Tendo la ndoa linatakiwa kuwa ni kitu cha kuleta starehe, lakini inakuwa vigumu kupata ashiki au kuwa karibu sana na mpenzi wako pale unapokuwa na tatizo la kushindwa kushiriki tendo la ndoa kutokana na wasiwasi. Tatizo la kushindwa kushiriki kufanya tendo la ndoa vizuri kutokana na wasiwasi ni kitu ambacho kinawaathiri watu wengi hasa wanaume. Kumekuwa na msukumo mkubwa katika jamii kuhusiana na uwezo wa kumudu kufanya tendo la ndoa na watu wamekuwa wakiuchukulia uwezo huo kama kigezo cha ukamilifu wa mwanamme.

Wasiwasi wa kushindwa kufanya tendo la ndoa ni kitu endelevu. Unaweza kumsababishia mwanamme kufika kileleni mapema, kumfanya mtu ashindwe kupata ashiki, na baadaye kusababisha mtu ashindwe kabisa kufanya tendo la ndoa. Mada yetu ya leo inazungumzia sababu za wasiwasi wa kufanya tendo la ndoa na suluhisho kwa tatizo hilo.

 

Utajuaje Kuwa Unashindwa Kufanya Mapenzi Kwa Sababu Ya Wasiwasi?

 

Watu wengi wamekuwa wakifikiri kuwa wana matatizo katika miili yao na kwamba wanahitaji tiba ya dawa wakati ambapo tatizo ni wasiwasi wao wa kufanya tendo la ndoa. Ili uweze kujua kwamba wewe ni mhanga wa tatizo hili au la, jiulize maswali yafuatayo:

1. Je, umekuwa unapata tatizo la jogoo kushindwa kuwika wakati ukiwa faragha na mpenzi wako, lakini ukiwa peke yako uume una uwezo wa kusimama kwa kujigusa mwenyewe ukiwa chumbani kwako na bila kuangalia picha za ngono?

2. Je, uume wako umekuwa ukisimama na kisha kusinyaa wakati fulani ukiwa na mwanamke – na hasa pale unapokutana na mwanamke huyo kwa mara ya kwanza au ya pili?

3. Umekuwa ukipata wasiwasi kuhusu uume wako kuwa tayari utakapokutana na mwanamke?

4. Umekuwa ukikwepa kufanya tendo la ndoa kwa wasiwasi kuwa pengine utashindwa kumridhisha mpenzi wako?

Kama majibu ni, ndiyo, kwa baadhi au kwa maswali haya yote, basi una tatizo la kushindwa kufanya tendo la ndoa kwa sababu ya kuwa na wasiwasi.

 

wasiwasi wa kufanya mapenzi
Wapenzi wengi wanaoshindwa kufika kileleni wanapojaribu kufanya mapenzi hawana sababu za msingi zinazotokana na udhaifu au matatizo katika miili yao. Bali wengi wao hushindwa kufanya mapenzi kutokana na wasiwasi walio nao kwamba watashindwa kumudu kulifanya tendo hilo. Wanashindwa kulikamilisha tendo hilo wakati hawana dosari kwenye sehemu zao nyeti. Tumeona kuwa wanaume wanaathirika kwa kushindwa kuwa tayari (uume kushindwa kusimama) ambapo kwa wanawake watashindwa kufika kileleni na kulifurahia tendo hilo.

 

Sababu Za Kushindwa kufanya Tendo La ndoa Kwa Kuwa Na Wasiwasi

 

Mtu anaposhindwa kufanya tendo la ndoa kutokana na wasiwasi kinachotokea ni kuwa mtu huyu anaacha kushiriki kikamilifu na mwenziwe. Mtu huyu anaacha kuweka akili yake kwenye mawazo ya kumpa ashiki na kutosikilizia vionjo vinavyoambatana na uwepo wake wa faragha wa yeye na mpenziwe. Badala ya kuwa na fikra za ashiki, anapeleka mawazo yake nje na kufikiria ni nini kitatokea iwapo atashindwa kulikamilisha tendo, ni vipi mwenziwe atamchukulia kuhusu urijali wake na jinsi mpenzi wake atakavyomchukulia kiujumla. Ataanza kupata wasiwasi kuwa kwa kuwa ana tatizo la jogoo kushindwa kuwika au kwa kukosa kufika kileleni basi mpenzi wake wa kike au wa kiume atamhesabu kuwa si mwanamme au mwanamke kamili.

Kupata ashiki kunaendana na kiwango cha utulivu wa ubongo wako. Hata kama mwenzi wako atakuvututia kwa kiwango gani, mijadala ndani ya ubongo wako kuhusu uwezo wako wa kumridhisha, itasababisha ushindwe kumudu kufanya tendo la ndoa kikamilifu.

Kwa wanaume, moja ya matokeo ya uwepo wa homoni za kuleta msongo wa mawazo (stess hormones) ni kuiminya mishipa ya damu. Damu itatiririka kwa kiwango kidogo sana kuelekea kwenye uume na kuufanya uume kushindwa kusimama imara. Hata uume wa mwanamme wa kawaida unaweza kushindwa kusimama na kuishia kupata tatizo hili.

Tatizo la kushindwa kufanya mapenzi kutokana na wasiwasi haliwasumbui sana wanawake ukilinganisha na wanaume, lakini linaweza kumzuia mwanamke kufikia utayari wa kufanya mapenzi. Wasiwasi unaweza kuzuia mwanamke asitokwe na ute wa kutosha wa kumfanya afurahie tendo la ndoa, na unaweza kuuzuia mwili wake kupenda kufanya mapenzi.

 

kushindwa tendo la ndoa

 

Tatizo la kushindwa kufanya mapenzi kutokana na wasiwasi ni la mzunguko usioisha kwa maana kwamba ukianza kuwa na wasiwasi kiasi cha kushindwa kufanya mapenzi, hali hiyo itakufanya uwe na wasiwasi zaidi na zaidi wa kulifanya tendo hilo.
Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha tatizo hili. Kwa kawaida, kama tatizo hili lilishawahi kujitokeza siku za nyuma, litachangia kwa kiasi kikubwa hali ya sasa hivi. Lakini, kwa kiwango kikubwa, tatizo la kushindwa kufanikisha tendo la ndoa kutokana na waswasi linatokana na wasiwasi wenyewe.

– Wasiwasi ya kuwa hutafanya vizuri na kushindwa kumridhisha mpenzi wako kitandani.

– Kuwa na wasiwasi kuhusu umbo lako la mwili, pamoja na unene wa kupindukia

– Matatizo katika mahusiano yenu

– Wasiwasi wa mwanamme kuwa uume wake ni mdogo

– Wasiwasi wa mwanamme wa kumaliza mapema au kuchukua muda mrefu mno kufika kileleni

– Wasiwasi wa mwanamke wa kushindwa kufika kileleni au kulifurahia tendo la ndoa
Mambo mengine yanayoweza kuchangia ni:

. Msukumo Wa Jamii

Msukumo wa jamii ni moja ya sababu kubwa za wasiwasi wa kufanya tendo la ndoa. Wanaume wanafikiri kuwa kushindwa kuwaridhisha wanawake kutawapunguzia mwonekano wao katika jamii na wanawake pia wanafikiri wanaume watawajadili kulingana na maungo yao na uwezo wao wa kufanya mapenzi. Hali hii inachochewa na jinsi watu wa karne hii wanavyoonyesha mambo ya siri hadharani na kulifanya tatizo hili kuwa kubwa zaidi kila siku.

 

mwanamke kushindwa kufanya mapenzi

 

. Kukosa Uzoefu

Kukosa uzoefu katika mapenzi kunaweza kusababisha matatizo madogomadogo katika kufanya tendo na baadaye kumsababishia mtu kupatwa na tatizo la kuwa na wasiwasi wa kufanya tendo la ndoa. Kuwahi kufika kileleni, kwa mfano, ni tatizo la kawaida kwa wale wasio na uzoefu wa kufanya mapenzi na likitokea husababisha aibu, na taratibu huanza kumjengea wasiwasi mhusika na baadaye kuishia na matatizo makubwa katika ufanyaji mapenzi.

. Kukutana Kimapenzi Kulikoleta Mtafaruku

Tendo la ndoa mtu hulifanya akiwa na matarajio. Kwa hiyo mtu ambaye aliwahi kugombana, kuwa na mabishano makubwa, au kuadhiriwa na mpenzi wake kwa sababu yo yote wakiwa chumbani anakuwa kwenye hatari kubwa ya kuwa na wasiwasi watakapokutana na mtu mwingine kimapenzi. Kwa kawaida watu wapo makini sana kuhusu uwezo wao wa kufanya mapenzi, miili yao n.k. na kitu cho chote kitakachowavuruga kuhusu haya, kitawaletea wasiwasi.

 

Namna Ya Kuondoa Wasiwasi Wa Kufanya Tendo La Ndoa

 

Wakati kila mmoja wa wahanga angependa kupata kitu cha kumwondolea tatizo hili mara moja, ukweli ni kwamba, kama ilivyo kwa wasiwasi wa aina nyingine, si swala la kulifanyia kazi kwa muda mfupi. Mtu ye yote anaweza kuondokana na tatizo hili, ila inahitajika juhudi, kujituma, na kuchukua hatua sahihi. Hapa chini ni baadhi ya hatua za kuchukua katika jitihada za kuondokana na tatizo hili:

. Kumweleza Mpenzi Wako Kuhusu Tatizo

Njia moja ambayo si sahihi katika kuepukana na tatizo hili ni kujaribu kupambana nalo bila kumwambia mpenzi wako. Hatua hii italifanya tatizo lako kuwa kubwa zaidi, na utakuwa kila wakati unayatuma mawazo yako kwenye kuchunguza kila kinachoendela kila wakati.

 

maandalizi katika mapenzi

 

Kuwa jasiri na kumwambia mwenzio kabla ya kuanza tendo la ndoa kwamba unasumbuliwa na wasiwasi wakati wa tendo na jinsi unavyojisikia. Uwezekano ni mkubwa sana kwamba mwenzi wako atakuelewa na kwa pamoja mtalifanyia kazi tatizo hilo.

. Jenga Upendo

Kimsingi, mtu uliye naye leo anaweza akawa ni mpenzi wako wa kudumu. Uzoefu – na hasa wa kuwa na mtu mmoja – ni tiba ya wasiwasi wa kufanya mapenzi. Hii inatokana na kuwa akili yako itakutuma kuamini kuwa, lo lote litakalokuwa, mwenzi wako bado ataendelea kuwa na wewe. Imani hiyo itakupunguzia woga ya kuwa wasiwasi wako wa kumudu kufanya mapenzi utakuja kukuharibia maisha yako.

. Ondoa Aibu Ya Kufanya Maandalizi

Wakati ambapo wanaume na wanawake wengi wanapata shida kushiriki maandalizi wakiwa na wasiwasi wa kufanya mapenzi, wengi bado wanaweza kujitahidi. Kiasi kikubwa cha wasiwasi kinakuwa kuhusu mwenzi anafurahia kwa kiasi gani tendo lenu. Unaweza kupunguza wasiwasi huu kwa kujitahidi kushiriki zaidi katika maandalizi, hivi kwamba, hata kama kiwango chako katika tendo hakikufikia pale mwenzi alipotegemea, bado utakuwa umemridhisha.

. Fanya mazoezi

Kuwa na kujiamini kimwili na nguvu za kutosha ni swala muhimu katika kuondoa wasiwasi wa kushindwa kufanya mapenzi kutokana na wasiwasi. Kadri unavyopunguza mawazo ya jinsi ulivyo au ya mwonekano wako, ndivyo utakavyoweza kushiriki tendo la ndoa bila ya kuwa na msongo wa mawazo. Fikiria mazoezi mazuri ya kuyafanya kama bado ulikuwa hufanyi, kuhakikisha kuwa unafikia hali ya juu ya kujiamini.

. Poteza Mawazo

Jaribu kuondoa mawazo ya kujifikiria na kuyarudisha kwenye shughuli iliyo mbele yako kwa kuweka muziki wa kimahaba au mkanda wa mapenzi wakati ukifanya mapenzi. Chagua kitu ambacho kinakuletea hisia. Kuondoa mawazo kutoka kwenye kulimudu tendo la ndoa kunaweza kukupunguzia wasiwasi unaokuzuia usipate ashiki.

 

kufanya maandalizi ya mapenzi

 

 

 

Usisite kuuliza swali lo lote kuhusiana na mada yetu ya leo na tunakaribisha maoni yako kuhusu mada hii. Tutafurahi sana kukujibu na kwa wakati.

 

Laurian.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii