Ujue Ugonjwa Na Tiba Ya UTI

 

ugonjwa wa uti

 

UTi ni ugonjwa ambao unasumbua watu wengi; watoto, vijana na watu wazima. UTI ni kifupisho cha Urinary Tract Infection. Huu ni ugonjwa ambao hushambulia figo (kidneys); ureters; ambayo ni mirija inayounganisha figo na kibofu cha mkojo, kibofu cha mkojo (bladder) na urethra; sehemu inayotoa mkojo toka kwenye kibofu cha mkojo hadi nje ya mwili. Kwa kifupu ugonjwa wa UTI hushambulia viungo vinavyohusika katika kupitisha mkojo kabla haujatoka nje ya mwili. Hebu tuvitazame viungo hivi kabla ya kueleza chanzo cha ugonjwa na tiba ya UTI baadaye hapa chini.

Kuelewa vizuri tunachokizungumzia hapa tazama picha ya viungo hivi na kwa kifupi hapa tutatoa maelezo ya picha hiyo. Figo ni viungo viwili vilivyopo kimoja kila upande wa uti wa mgongo eneo la kiunoni. Figo hufanya shughuli nyingi katika mwili wa binadamu ikiwepo ya kutoa uchafu na maji ya ziada katika damu, na huvitoa vitu hivi kama mkojo. Kwa sababu hii, figo ni muhimu sana katika kuweka msukumo wa damu kwenye kiwango kizuri. Figo pia husikia
mapema sana mabadiliko ya kiwango cha sukari mwilini na mabadiliko katika kiwango cha msukumo wa damu (blood pressure). Kiwango cha sukari na msukumo wa damu vikizidi, vyote huweza kuleta madhara kwenye figo.

 

UTI

 

 

Ureters ni mirija miwili myembamba yenye urefu wa yapata nchi 10 hivi kila mmoja ambayo huchukua mkojo kutoka kwenye figo na kuumwaga ndani ya kibofu cha mkojo.

Kibofu cha mkojo ni kijimfuko kidogo kinachopokea mkojo kutoka kwenye mirija ya ureters na kuuhifadhi. Mkojo ukifikia kiwango fulani ndani ya kibofu cha mkojo, tunasikia haja ya kuupunguza (kukojoa) na ndipo misuli ya nje ya kibofu cha mkojo hujibana na kuukamua mkojo nje ya kibofu.

Urethra ni mrija unaounganisha kibofu cha mkojo na nje ya mwili.

Sehemu yo yote katika hizi tulizozitaja hapa juu, inaweza ikapata maambukizi ya UTI na kadri maambukizi hayo yatakavyokuwa ndani zaidi ukitokea nje, ndivyo ugonjwa huu utakavyokuwa umefikia hali mbaya zaidi. Wasichana na akina mama hupata maambukizi haya kwa wingi zaidi kuliko wavulana au akina baba. Asilimia kama 40 ya wanawake na asilimia 12 ya wanaume hupata maambukizi haya ya UTI katika maisha yao.

 

Chanzo Cha UTI Ni Nini?

 

 

Mkojo kwa kawaida ni kitu kisicho na wadudu wo wote wabaya. Maambukizi yanakuja pale wadudu wanapoingia kwenye mkondo wa mkojo kupitia kitundu cha kutolea mkojo nje ya mwili na kufuata mkondo huo kuelekea kwenye figo. Wadudu hao wakisha ingia huanza kuzaliana. Asilimai 90 ya maambukizi yasiyo mabaya sana huwa ni ya bacteria waitwao Escherichia Coli au kwa kifupi E. Coli. Kwa kawaida bacteria hawa huishi katika utumbo au karibu na maeneo ya mkundu. Wadudu hawa wanaweza wakatembea kutoka eneo la mkundu wakaelekea kwenye tundu la mkojo na kuingia. Lakini, kutojisafisha kwa namna nzuri (kwa mfano, kutawadha kuanzia nyuma kuja mbele) au ngono ndizo njia mbazo huambukiza
bacteria hawa kirahisi zaidi.

 

bacteria wa UTI  - E. Coli

Bacteria wa E.Coli

 

Wanawake hupatwa zaidi na maambukizi haya kwa sababu ya ukaribu wa mkundu na kijitundu cha kutolea mkojo na kwa sababu ya ufupi wa urethra katika miili yao ukilinganisha na wanaume. Wanawake wanaoshiriki ngono mara nyingi na watu tofauti hupatwa na maambukizi zaidi kuliko wale wanaoshiriki kwa kiwango kidogo.

Wanawake wanaotumia diaphragms kama njia ya uzazi wa mpango hupatwa zaidi na tatizo hili pia akina mama waliokoma hedhi kwa sababu ya ukosefu wa homoni ya estrogen. Kukosekana kwa estrogen kunasababisha mabadiliko katika mkondo wa mkojo na kuufanya uweze kuambukizwa kwa urahisi zaidi.

Matatizo yo yote yanayosababisha mkojo usitoke nje kwa urahisi huongeza uwezekano wa kupata maambukizi ya UTI. Mifano ni; watoto kuzaliwa na matatizo katika mikondo yao ya mkojo ambayo huzuia mkojo usitoke nje kirahisi, matatizo ya kidney stones na prostate kukua kupita kiasi; na watu wanaotoa mkojo kupitia kifaa maalumu (catheter).

Tendo la kukojoa huwatoa bacteria hawa nje ya mwili lakini wakiwa wengi sana, kukojoa hakuwezi kuwatoa wakaisha. Wadudu hawa husafiri kwenye urethra hadi kwenye kibofu cha mkojo ambako watazaliana. Wanaweza kuendelea kusafiri kupitia ureters hadi kwenye figo ambako pia watazliana na kuleta matatizo makubwa endapo tiba nzuri haitatolewa kwa wakati muafaka.

 

Ni Nini Dalili Za UTI?

 

 

Dalili za ugonjwa huu huwa tofauti kulingana na hatua ambayo ugonjwa umeshafikia.

 

maumivu ya UTI

 

Lower UTI ni hatua ya ugonjwa kushambulia maeneo ya urethra na kibofu cha mkojo (bladder). Katika hatua hizi, mgonjwa atasikia dalili zifuatazo:

. Maumivu wakati wa kukojoa
. Kujisikia kukojoa mara kwa mara lakini kutoa mkojo kidogo tu
. Damu katika mkojo
. Mkojo wenye rangi ya chai
. Mkojo wenye harufu kali
. Maumivu ya kiuno kwa wanawake
. Maumivu ya sehemu za nyuma kwa wanaume

Upper UTI ni maambukizi ya ndani ya figo. Hii ni hatua mbaya sana endapo bacteria wataanza kuingia kwenye mkondo wa damu kutoka kwenye figo – SEPSIS. Sepsis huweza kusababisha msukumo wa damu kuwa mdogo sana (Low Blood Pressure), mshituko au kifo.

Dalili za upper UTI ni:

. Maumivu ya maeneo ya juu ya mgongo
. Homa
. Kusikia baridi
. Kusikia kichefuchefu
. Kutapika

 

Hatua Za Kujikinga Na UTI

 

Kuna hatua unazoweza kuchukua ili usipatwe na maambukizi ya ugonjwa huu kirahisi. Hii ni pamoja na kujifuta au kutawadha ukianzia mbele kwenda nyuma baada ya haja kubwa au ndogo. Kunywa maji mengi, glasi 6 hadi 8 za maji kila siku na kuhakikisha unakunywa maji baada ya kushiriki tendo la ndoa. Haifai kuubana mkojo kwa muda mrefu, timiza haja mara itokeapo. Kusafisha maeneo nyeti mara kwa mara. Kuoga kupitia bomba la mvua ni bora zaidi kuliko kutumbukia kwenye josho. Ni vema kuvaa chupi zilizotengenezwa kwa pamba.

 

Tiba Ya UTI

 

Tiba kwa ugonjwa wa UTI kwa hatua zote ni antibiotics. Daktari ataamua kukupa tiba na kukuruhusu kuendelea na tiba nyumbani kwako au kukulaza kulingana na alivyoiona hali ya ugonjwa wako. Tiba ya lower UTI ikitolewa kwa wakati mwafaka na inavyotakiwa, hakuna matatizo makubwa yanayoweza kutokea.

 

Dawa ya UTI

Dawa ya UTI. Bonyeza Juu Ya Picha Kusoma Maelezo

 

Lakini tiba ispotolewa kwa wakati, maambukizi haya ya mkondo wa mkojo huweza kuleta matatizo makubwa. Pamoja na mengine mgonjwa anaweza:

. Kupata maambukizi ya mara kwa mara
. Kupata uharibifu wa figo wa kudumu  na kuhitaji  huduma maalumu ya kutibu  figo  (dialysis).
. Kutokea uwezekano wa kuzaa watoto wenye uzito mdogo au wanaozaliwa kabla ya wakati.                                                                                        . Wanaume wanaougua UTI mara kwa mara wanakuwa kwenye hatari ya kupata madhara kwenye tezi dume (prostatitis). Uvimbe huweza kutokea kwenye tezi dume na kusababisha maumivu wakati wa haja ndogo au kutoa shahawa.                                                                               . Sumu katika damu. Mara chache huweza ikatokea kuwa bakteria wakasambaa kutoka ndani ya figo na kuingia kwenye mfumo wa damu (sepsis) na baadaye kusambaa hadi kwenye viungo vingine muhimu vya mwili. Hali hii ikitokea, itabidi mgonjwa awekwe chini ya uangalizi mkali wakati akipewa tiba ya kuwaua bakteria hao.

Katika mada nyingine tutatazama tatizo la high blood pressure .
Usisite kuuliza swali au kutoa maoni yako kuhusiana na mada yetu. Tutafurahi sana kusikia kutoka kwako na kukujibu.

 

Kwa maelezo zaidi na ya kina, tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu hapa chini kwa kujaza fomu, au tutumie barua pepe kupitia promota927@gmail.com au tupigie simu kwa namba zifuatazo: 0655 858027 au  0756 181651.

 

Jina Lako

Anuani Ya Barua Pepe

Namba Yako Ya Simu

Kichwa Cha Habari

Swali Au Maoni Yako

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii

404 Not Found

404 Not Found


nginx/1.10.3