Kisukari, Unajua Chanzo Na Tiba Yake?

aina za kisukari

 

Kisukari ni kundi la magonjwa yanayohusiana na ufanyaji kazi wa mwili ambapo mtu anakuwa na kiwango kikubwa cha sukari aina ya glucose katika mwili kutokana na  mwili wake kukosa uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha au seli za mwili wake haziwezi kutumia insulin iliyopo au pengine mwili kuwa na matatizo yote mawili kwa pamoja. Mgonjwa wa kisukari hupata haja ndogo mara kwa mara (polyuria), kusikia kiu kila wakati (polydipsia) na njaa (polyphagia).

Kuna aina tatu za kisukari; Type 1 Diabetes, Type 2 Diabetes na Gestational Diabetes.

 

1. Type 1 Diabetes

 

Mwili wa mgonjwa wa aina hii ya kisukari hautengenezi insulin kabisa. Kisukari cha aina hii mara nyingine huitwa insulin-dependent diabetes, juvenile diabetes, au early-onset diabetes. Watu huwa na kisukari aina hii wanapokuwa na umri wa chini ya miaka 40 na hasa katika miaka ya mwanzo kabisa ya ujana wao. Kisukari cha aina hii huwapata watu wachache ukilinganisha na aina nyingine za kisukari, karibu asilimia 10 tu ya wagonjwa wote wa kisukari huwa na aina hii ya kisukari.

Mgonjwa mwenye kisukari cha aina hii atapaswa kutumia sindano za kumwongezea insulin mwilini katika maisha yake yote na lazima kila wakati ahakikishe kuwa kiwango chake cha sukari mwilini kinakuwa sawa kwa kuchukua vipimo na kufuata mpango wa chakula maalum.

 

2. Type 2 Diabetes

 

Mwili hautengenezi insulin kwa kiwango cha kutosha au seli za mwili zinashindwa kuitumia insulin iliyopo (insulin resistance). Karibu asilimia 90 ya wagonjwa wa kisukari katika ulimwengu husumbuliwa na aina hii ya kisukari.

Watu wenye unene usio wa kawaida na wenye uzito mkubwa wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kisukari cha aina hii ukilinganish na wale wenye miili ya kawaida. Kuwa na uzito mkubwa au unene usio wa kwaida husababisha mwili kutoa kemikali zinazovuruga mfumo wa namna ya mwili unavyotumia chakula kilichoyeyushwa ili kuupa mwili nguvu na kuuwezesha kukua.

Kuwa na uzito mkubwa, kutofanya mazoezi na kutozingatia namna ya kula chakula kinachofaa, humweka mtu katika hatari kubwa ya kupata aina hii ya kisukari . Kwa mfano, kunywa soda moja tu kwa siku kunaongeza uwezekano wa kupata aina hii ya kisukari kwa kiwango kikubwa sana.

Hatari ya kupata kisukari cha aina hii huongezeka pia na umri, sababu kamili haijajulikana bado lakini labda kwa vile umri ukiongezeka mtu huongezeka uzito na hupunguza shughuli za kuutumia mwili wake.

Inaonekana pia kuwa mtu mwenye ndugu wa karibu mwenye ugonjwa huu, naye pia huweza kuupata ugonjwa huu. Watu wa asili ya Mashariki Ya Kati, Afrika na kusini mwa mwa Bara la Asia hupatwa sana na kisukari cha type 2 Diabetes.

Kuwa na kiwango kidogo cha homoni ya testosterone kumeonyesha kuwa na mchango katika kusababisha aina hii ya kisukari. Wataalamu wanasema kuwa kuwa na kiwango kidogo cha testosterone katika mwili kunahusiana na tatizo la mwili kutoweza kuitumia insulin (insulin resistance).

Kuna baadhi ya watu ambao wameweza kuudhibiti ugonjwa huu kwa kupunguza uzito wa miili yao, kufuata mipango mizuri ya chakula, kufanya mazoezi ya miili yao na kuchukua vipimo vya mara kwa mara kujua viwango vya sukari katika miili yao. Lakini kisukari cha aina hii ya pili ni ugonjwa unaokua kila siku na dalili zake kuongezeka kila siku, hivyo mwishowe mgonjwa itabidi aongezewe insulin. Mara nyingi wagonjwa wa aina hii ya kisukari mwishowe huongezewa insulin ya vidonge.

 

 3. Gestational Diabetes

 

Hiki ni kisukari wanachopata wanawake wakati wanapokuwa wajawazito. Baadhi ya wanawake wanakuwa na viwango vikubwa sana vya glucose katika damu zao na miili yao haina uwezo wa kutengeneza insulin ya kutosha kuweza kusafirisha glucose hiyo hadi kwenye seli za miili yao hivyo kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika miili yao.

Kisukari hiki huweza kudhibitiwa vizuri kwa kula chakula kinachofaa na kufanya mazoezi, Ni asilimia ndogo kati yao ambao huhitaji kupewa dawa. Gestational diabetes isipodhibitiwa huweza kusababisha matatizo wakati wa uzazi au kufanya mtoto anayezaliwa kuwa mkubwa kuliko alivyostahili.

 

madhara ya kisukari

 

Kisukari Ni Tatizo La Matumizi Ya Chakula Mwilini

 

Kisukari (diabetes mellitus) huhesabiwa kama ni tatizo la matumizi ya chakula katika mwili. Mwili wa binadamu hutumia chakula kilichoyeyushwa ili kuuwezesha kuwa na nguvu na kukua. Chakula cha aina nyingi tukilacho huvunjwavunjwa na kupata glucose, aina ya sukari katika damu ambayo ndiyo chanzo kikuu cha nguvu katika mwili wa binadamu.

Chakula baada ya kuyeyushwa, glucose huingia katika mfumo wa damu. Seli za mwili hutumia glucose hiyo ili kupata nguvu na kukua. Lakini seli haziwezi kuchukua glucose hiyo bila uwepo wa insulin, insulini ndiyo inayoziwezesha seli hizo kuchukua glucose.

Insulin ni homoni inayotengenezwa na kongosho. Baada ya kula, kongosho hutoa insulin ya kutosha kuwezesha seli kuchuka glucose iliyopo katika damu, na mara baada ya glucose hiyo kuchukuliwa na seli, kiwango cha sukari katika damu hushuka.

Mtu mwenye kisukari ni yule ambaye kiwango chake cha glucose katika damu ni kikubwa mno (hyperglycemia) kutokana na kwamba mwili wake hautengenezi insulin, hautengenezi insulin ya kutosha au seli kushindwa kuitumia insulin inayotengenezwa na kongosho. Mapato yake ni kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika damu ambayo baadaye hutolewa nje ya mwili kupitia katika mkojo. Mgonjwa wa kisukari ana zahana kubwa ya glucose katika damu yake lakini mwili unashindwa kuitumia glucose hiyo kwa matumizi yake ili upate nguvu na kukua.

Katika kurasa zifuatazo tutaona dalili za kisukari na madhara yanayotokana na kuwa na ugonjwa huo, chakula na mazoezi kwa mtu mwenye kisukari na mwisho tiba ya mtu mwenye kisukari kwa kutumia insulin.

Ndugu msomaji wetu tunakuomba usisite kutuuliza maswali au kutoa maono yako kuhusu mada hii. Tutafurahi sana kukujibu au kupokea maoni yako.

 

Ukurasa      1    2    3     4

 

 

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii

404 Not Found

404 Not Found


nginx/1.10.3