Mzunguko Wa Hedhi. Utaijuaje Siku Bora Ya Kupata Mimba?

 

mzunguko wa hedhi

 

Watu wengi tunafahamu kuwa mzunguko wa hedhi wa mwanamke ni siku 28 na misemo mingi imekuwa ikitumika ikihusisha mzunguko huo na mwezi wa kalenda wa mwaka. Misemo kama kwenda mwezini, kuingia mwezini n.k. ni ya kawaida kuisikia. Jee, ulishawahi kudadisi uhusiano wa siku 29.5 za mwezi na mzunguko huu wa hedhi unaochukua siku 28? Kama bado, hapa kuna nadharia fupi:

Kama inavyojulikana kuwa jua na mwezi vina mchango katika maisha ya mimea na binadamu, homoni za binadamu hutolewa mwilini kulingana na kiwango cha mwanga wa mwezi. Kabla ya ugunduzi wa umeme, utendaji kazi wa miili ya binadamu ulitegemea sana kiwango cha mwanga wa mwezi. Na akina mama wote walipata hedhi kwa wakati mmoja. Maisha ya sasa ambapo kuna vyanzo vingi vya mwanga usiku na mchana, mizunguko ya hedhi ya akina mama haiendani tena na uwepo wa mwanga wa mwezi.

Lakini hedhi ni nini na kuna uhusiano gani kati ya mzunguko wa hedhi wa mwanamke na siku za kubeba mimba mwanamke au kwa maneno mengine, katika mzunguko huo ni zipi siku ambazo mwanamke anaweza kupata mimba? Hayo ndiyo maswali ambayo tutayajibu katika mada hii.

 

Ni Nini Kinachotokea Katika Siku 28 Za Mzunguko Wa Hedhi?

 

Mwanamke anapokwenda mwezini kwa mpango unaojirudia na unaotabirika, tunauiita mzunguko wa hedhi. Mzunguko wa hedhi ni mfululizo wa mabadiliko katika mwili wa mwanamke katika kujiandaa kwa mimba ambayo inaweza ikatungwa. Kila mwezi ovari zinaachia yai moja lililokomaa (ovulation) na homoni katika mwili hubadilika kila wakati ili kuiandaa nyumba ya uzazi (uterus) kwa mimba itakayotungwa. Endapo yai lililoachiwa halitarutubishwa, ile ngozi nyororo inayotanda juu ya nyumba ya uzazi hujinyofoa na kutoka nje ya uke, na tendo hili ndilo linaloitwa hedhi (menstruation).

Kuwa na mzunguko wa hedhi unaoeleweka ni ishara kuwa viungo muhimu katika mwili wa mwanamke vinafanya kazi vizuri.
Mzunguko wa hedhi huhesabiwa kutoka siku ya kwanza ya kuanza kutoa damu (period) hadi siku ya kwanza ya kutoa damu ya mwezi unaofuata.

Mzunguko wa hedhi huchukua wastani wa siku 28 lakini kila mwanamke ana tofautiana na mwingine. Mizunguko ya mwezi
huweza kuchukua kati ya siku 21 hadi 35. Msichana anapoanza kupata hedhi mizunguko yake huwa mirefu, isiyotabirika – na si ajabu akakosa kupata siku zake kwa kipindi fulani. Kadri umri wake unavyoongezeka, mizunguko yake hupungua siku na kuwa mifupi na inayotabilika zaidi.

 

elimu ya mzunguko wa hedhi

 

 

Mzunguko wa mwezi wa mwanamke unaweza kujirudia kwa vipindi vilivyo sawa – au vilivyo na urefu wa siku tofauti, damu inaweza kutoka kwa wingi au kidogo, ikaambatana na maumivu au isiwe na maumivu. Vyote hivi ni vitu vya kawaida kwa mwanamke, – “mzunguko wa kawaida kwa mwanamke ni ule aliouzoea.” Tunasema kuna mabadiliko au kuna matatizo katika mzunguko wa hedhi wa mwanamke pale mambo yanapokwenda tofauti na alivyoyazoea mwanamke mwenyewe katika mwili wake. Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha kuvurugika kwa mzunguko wa mwezi wa mwanamke. Baadhi ya sababu hizo ni kama zifuatazo:

Kubadili Njia Ya Mpango Wa Uzazi: Kubadili njia ya mpango wa uzazi kutoka moja hadi nyingine kunaweza kuvuruga mzunguko wa hedhi.

 
Kukosa Uwiano Wa Homoni: Ni kawaida kwa mwanamke kukosa uwiano mzuri wa homoni za estrogen na progesterone miaka michache baada ya kuvunja ungo na kabla ya kukoma hedhi. Hali hiyo huweza kusababisha mzunguko wa hedhi kuwa mrefu au mfupi na kutokwa na damu kidogo au nyingi kupita kiasi wakati wa hedhi.

 
Ujauzito Au Kunyonyesha: Kuchelewa kupata au kukosa hedhi ni dalili ya awali ya ujauzito. Kunyonyesha kwa kawaida humzuia mwanamke kurudia kuanza kupata siku zake baada ya mimba.

 
Matatizo Ya Ulaji, Mazoezi Mazito Au Kupungua Mwili: Matatizo katika ulaji wa chakula, kupungua uzito kwa kiwango kikubwa na kuongezeka kwa shughuli nzito za mwili huweza kusimamisha mzunguko wa hedhi.
Polycystic Ovary Syndrome (PCOS): Hii ni hali inayoweza kutokea ambapo vifuko vidogo vilivyojaa majimaji (cysts) huota kwenye ovari.  Dalili ya Polycystic ovary syndrome ni kupata hedhi zisizotabilika au hedhi fupi au kukosa kabisa hedhi. Hii ni kwa sababu mwanamke mwenye PCOS hawezi kutoa yai (ovulation) kila mwezi kama inavyotakiwa. Utengenenezaji wa homoni zake unaweza kuwa hauna uwiano unaotakiwa, na pengine kukawa na kiwango kikubwa mno cha testosterone.

 
Ovari Kuacha Kufanya Kazi Mapema – Premature Ovarian Failure: Hili ni tatizo ambapo ovari huacha kufanya kazi kama inavyotakiwa kwenye umri unaopungua miaka 40. Wanawake wenye tatizo hili huweza kuwa na siku ambazo hazitabiriki kwa kipindi kirefu cha maisha yao.

 
Pelvic Inflammatory Disease (PID): Maambukizi ya wadudu kwenye viungo vya uzazi huweza kumsababishia mwanamke apate hedhi zisizotabirika.

 
Uterine Fibroids: Uvimbe ulioota katika nyumba ya uzazi husababisha damu kutoka kwa wingi wakati wa hedhi na
kutokwa damu katikati ya hedhi.

 
Matatizo Ya Tezi Ya Thyroid: Tezi ya thyroid ambayo hupatikana katika eneo la shingo la binadamu hutoa homoni za kusimamia mwenendo wa kemikali zinazobadili chakula na kuleta nguvu katika mwili. Mabadiliko ya kiwango cha thyroid – kuwa na kiwango kidogo cha thyroid (hypothyroidism) katika mwili – huweza kusababisha kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi.

 
Kipindi hiki cha mzunguko huu wa hedhi kinagawanyika katika awamu nne zinazoongozwa na kupanda na kushuka kwa homoni katika mwili. Mwanamke kwa wastani hupitia mizunguko ya hedhi 450 katika maisha yake. Hapa chini tutaziona awamu hizo nne na kuelezea ni nini kinachotokea katika mwili wake katika kila awamu. Hapa chini tunazijadili awamu hizo nne za mzuguko wa hedhi:

 

Hedhi-Kumwaga Damu (The Bleeding Phase)

 

Hedhi (menstruation) ni tendo linalotokea kila mwezi kwa mwanamke ambalo linahusisha utokwaji wa damu na vitu
vingine vilivyokuwa vinajijenga kwenye tumbo la uzazi, kupitia sehemu ya uke.

Msichana wa kawaida huanza kupata siku zake akiwa na umri wa miaka 12, hii ni wastani na haina maana wote wataanza kupata siku katika umri huo. Wapo wasichana wanaoanza kuona siku zao kwenye umri mdogo sana wa miaka 8 na wapo wanaochelewa hadi kwenye umri wa miaka 15. Mara nyingi wasichana huanza kuona siku zao miaka 2 baada ya maziwa (matiti) kuanza kuota.

 

mwanamke na hedhi

 

Mwanamke anapoingia mwezini, utando uliokuwa umejijenga kuzunguka nyumba ya uzazi (uterus) pamoja na damu ya ziada
hutoka nje ya mwili kupitia sehemu ya uke. Utokaji huo wa vitu hivi unaweza kuwa unaolingana kila mwezi au ukawa tofauti mwezi hadi mwezi. Utokaji huo huweza kuwa tofauti kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine. Damu inaweza kutoka kwa kiasi kidogo au nyingi na urefu wa hedhi (siku za kutoka damu) zinaweza kuwa tofauti kutoka mwezi mmoja hadi mwingine. Kwa kawaida mwanamke hutokwa damu kwa siku 3 hadi 5, lakini siku 2 hadi 7 bado inachukuliwa kuwa ni kawaida.

Mada hii ni ndefu, hivyo  basi katika kuijadili tumeigawa katika  kurasa tano. Ukurasa unaofuta utazungumzia kwa undani kuhusu awamu za mzunguko wa hedhi wa mwanake na kufuatiwa na ukurasa utakaozungumzia sababu za mwanamke kukosa mtoto na ugumba wa mwanamme. Ukurasa wa nne utazungumzia sababu za ugumba kwa mwanamme na mwanamke na mwisho tutaona tiba ya ugumba kwa mwanamke.

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.

Ukurasa        1                 3            4          5

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii