Homa Ya Ini: Hepatitis C

 

hepatitis B

 

Baada ya kujadili kuhusu hepatitis A na B katika kurasa zilizotangulia, leo tutaona aina nyingine ya homa ya ini, Hepatitis C. Kama ilivyo kwa hepatitis A na B, ugonjwa huu husababishwa na aina nyingine ya kirusi aitwaye Hepatitis C virus (HCV). Ni vigumu kwa kinga za mwili kuuondoa ugonjwa huu, hivyo ugonjwa huu mara nyingi huwa ni wa muda mrefu (chronic). Asilimia 85 ya watu wanaopatwa na hepatitis C, wanashindwa kuuondoa kwa kinga zao za mwili. Baada ya muda mrefu, ugonjwa huo huharibu kabisa maini na kusababisha yashindwe kabisa kufanya kazi. Kitu kibaya ni kwamba virusi hawa wakiingia mwilini, hakuna dalili zo zote za awali zitakazojitokeza.

Kirusi wa hepatitis C hana uhusiano kabisa na virusi wengine wanaosababisha homa ya ini, kama hepatitis virus A au hepatitis virus B. Kirusi wa hepatitis C anatoka kwenye familia ya virusi ya Flaviviridae. Virusi wengine kutoka kwenye familia hii ni wale wanaoleta magonjwa ya homa ya manjano na dengue.

Uwepo wa virusi wa hepatitis C mwilini huzishtua kinga za mwili zianze kufanya kazi na hivyo uvimbe hutokea. Baada ya miaka kumi, ishirini au zaidi, uvimbe huu huweza kujenga makovu (cirrhosis). Maini yakisha fikia kuwa na cirrhosis yanaweza kushindwa kufanya kazi zake inavyopaswa hali inayoweza kupelekea madhara makubwa na hata kifo. Na, maini yenye cirrhosis yanaweza kupata saratani kwa urahisi zaidi.

 

Dalili Za Hepatitis C

 

Asilimia 75 ya wagonjwa wa hepatitis C hawapati dalili zo zote wanapoambukizwa HCV. Asilimia 25 inayobakia wanaweza kuona dalili zifuatazo:

. uchovu
. kukosa hamu ya kula
. maumivu ya misuli
. homa

Mara chache mgonjwa ataona mabadiliko ya rangi ya ngozi au macho (kuwa njano) kwenye hatua hii.

Baada ya muda, mgonjwa ataanza kuona matokeo ya kuwa na uvimbe wa muda mrefu uliotokana na kinga za mwili kujaribu kuwaondoa virusi wa hapatitis C. Wakati cirrhosis ikijijenga, mgonjwa anaweza kuona yafuatayo:

. udhaifu wa mwili
. kukosa hamu ya kula
. kukonda
. maziwa kukua kwa wanaume (gynecomastia)
. vipele kwenye viganja
. damu kutoganda upesi ukiumia

Maini hatimaye hushindwa kuendelea kufanya kazi cirrhosis ikikomaa, hali ambayo ni hatari kwa maisha ya mgonjwa. Mgonjwa anaweza kuchanganyikiwa au kuzirai (coma) kwa vile maini yatashindwa kuondoa baaadhi ya sumu nje ya mwili.

Kuongezeka kwa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu ya maini (portal hypertension) kunaweza kusababisha maji kujaa ndani ya tumbo na hatimaye kupelekea kuvimba kwa veni za kwenye koromeo ambazo zitachubuka kirahisi na kusababisha damu nyingi kuvuja. Kuongezeka huku kwa msukumo wa damu kwenye mishipa ya maini kunaweza kusababisha figo kufeli au kuvimba kwa bandama.

Pamoja na kusababisha damu ishindwe kuganda kwenye majeraha, hepatitis C iliyokomaa hufanya rangi ya ngozi na macho kugeuka na kuwa njano (jaundice) kwa sababu maini hayawezi tena kuondoa mchanganyiko wa vitu vya njano (bilirubin) unaotokana na chembe chembe nyekundu za damu zilizozeeka.

 

Hepatitis C Inaenezwaje?

 

Njia kuu ya kuenea kwa hepatitis C ni kupitia damu yenye virusi wa hepatitis C:

. Kuchangia sindano baina ya watumiaji wa madawa ya kulevya
. Kuchomwa sindano na wahudumu wa afya ambazo kwa bahati mbaya hazikuwa salama
. Mtoto kupata ugonjwa huu kutoka kwa mama yake anapozaliwa
. Kujamiiana bila kutumia kinga
. Kutumia vifaa vya kutobolea ngozi visivyo salama

 

Tiba Ya Hepatitis C

 

Virusi wa hepatitis C wapo wa makundi madogo tofauti yapatayo 6 na kila kundi lina usikivu tofauti kwa aina ya tiba itakayotolewa. Hali hii huifanya tiba ya hepatitis C kuwa na changamoto kwani inatakiwa uchunguzi wa kina kufanyika ili kujua aina halisi ya kirusi aliyo nayo mgonjwa ili apewe tiba anayostahili.

Kwa miaka mingi mchanganyiko wa sindano za interferon na vidonge vya ribavirin umekuwa ukitumika. Tiba hii imekuwa na mafanikio kwa karibu asilimia 60 tu ya wagonjwa. Tiba hii pamoja na kuwa haipatikani kwenye baadhi ya nchi, watu wengi wanaopata tiba hii hawamalizi dozi.

Maendeleo ya kisayansi yamewezesha kugundulika kwa dawa mpya ambazo tayari zimepasishwa na FDA na nyingine bado zinaendelea kugunduliwa, dawa ambazo wagonjwa wanaweza kuvumilia kuzitumia. Mfano wa dawa hizi ni mchanganyiko wa Telaprevir na boceprevir, Sofosbuvir (iliyopasishwa 2013) na Ledipasvir ya 2014.

Katika ukurasa wa mwisho wa mfululizo wa mada yetu ya ugonjwa wa homa ya ini, tutajadili homa ya ini ya hepatitis D na hapatitis E.

 

Usisite kutuandikia ili kutoa maoni yako kuhusu mada hii, tutafurahi kupata mchango wako na kuona kuwa tumekujibu.

 

Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.

 

Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.

 

Ukurasa       1             2             3         4

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii