Vidonda Vya Tumbo, Ugonjwa Huu Ni Nini?

Vidonda vya tumbo (Peptic Ulcers) ni ugonjwa unaompata mtu ambapo kunatokea vijitundu au michubuko katika kuta za ndani za viungo vya mfumo wa uyeyushaji chakula. Michubuko hiyo huweza kutokea katika eneo la mfuko wa tumbo, katika duodenum au katika eneo la koo. Inakadiriwa kuwa asilimia 5 hadi 10 ya watu hupatwa na ugonjwa huu angalau mara moja katika maisha yao. Huu ni ugonjwa ambao unaweza kumrudia mtu baada ya kupona endapo chanzo chake hakikudhibitiwa. Kama ugonjwa huu utamrudia mgonjwa , mtu huyu atakuwa amejiweka kwenye hatari kubwa ya kupata madhara makubwa zaidi kama kutokwa na damu au kutokea tundu kubwa katika kuta za mfuko wa tumbo.

 

 Chanzo Cha Vidonda Vya Tumbo

 

Bacteria: Chanzo kikubwa cha ugonjwa wa vidonda vya tumbo ni bacteria waitwao Helicobacter pylori (H. pylori). Bacteria hawa huenezwa kwa kula chakula na kunywa maji. Katika mwili wa binadamu bacteria hawa wapo katika mate na katika ute unatanda juu ya kuta za duodenum na mfuko wa tumbo.

wadudu wa vidonda vya tumbo

H pylori hutengeneza enzyme (urease) ambayo hupunguza makali ya tindikali katika tumbo. Hilo likitokea, tumbo hutengeneza tindikali zaidi na hii ndiyo husababisha michubuko katika kuta za tumbo na duodenum. Bacteria hawa pia hudhoofisha kinga ya tumbo na kusababisha maumivu mbalimbali. Kwa sababu bacteria hawa wapo katika mate ya mgonjwa huyu, njia moja ya maambukizi ya ugonjwa huu ni tendo la kubadilishana mate wakati wa kubusiana.

Madawa: Matumizi ya madawa husababisha vidonda vya tumbo. Dawa nyingi ambazo huweza kusababisha vidonda vya tumbo ni zile za kupunguza maumivu ya kichwa na maumivu mengine madogo madogo. Dawa hizo ni kama aspirin, diclofenac, naproxen, ibuprofen n.k. Dawa hizi hupunguza uwezo wa tumbo wa kutengeneza utando wa ute wa kulikinga tumbo hivyo kulifanya liweze kuliwa kirahisi zaidi na tindikali. Daw hizi pia hupunguza mtiririko wa damu kuelekea kwenye eneo la tumbo hivyo kupunguza uwezo wa tumbo wa kukarabati seli zilizoharibika.

 Urithi: Ugonjwa huu wa vidonda vya tumbo umeonyesha kuwa ni wa kurithishwa kwani wagonjwa wengi walibainika kuwa na ndugu wengi ambao wanaugua pia ugonjwa huu.

 Pombe Na Tumbaku: Watu wanaokunywa pombe na wale ambao wanatumia tumbaku wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kuupata ugonjwa huu wa vidonda vya tumbo.

 Msongo Wa Mawazo: Haijabainishwa moja kawa moja kwamba msongo wa mawazo unaweza kusababisha vidonda vya tumbo, bali mtu mwenye vidonda vya tumbo atakuwa na hali mbaya zaidi pale atakapokuwa na msongo wa mawazo.

 

Dalili Za Vidonda Vya Tumbo

 

Maumivu Ya Tumbo: Dalili ya kwanza kabisa ya ugonjwa huu ni maumivu ya tumbo ambayo yanaongezeka pale tindikali inapogusa eneo lililoathirika. Maumivu haya yanaweza kutokea sehemu yoyote kuanzia eneo la kitovuni hadi kwenye mifupa ya mabega na yanaweza kuchukua muda mfupi au kuendelea kwa saa chache. Maumivu husikika zaidi wakati tumbo ni tupu na huwa makali zaidi nyakati za usiku. Maumivu hupungua kwa muda mfupi baada ya kula chakula. Mgonjwa anaweza kupata nafuu kwa siku au wiki chache halafu maumivu hurudi tena.

vidonda vya tumbo

Madhara Ya Vidonda Vya Tumbo

 Matatizo Wakati Wa Kumeza: Mtu mwenye vidonda vya tumbo hupata matatizo pale anapojaribu kumeza chakula au hujisika vibaya mara baada ya kupata chakula.

 Kutapika: Dalili nyingine ya tatizo la vidonda vya tumbo ni kujisikia kutapika au kutapika baada ya kupata chakula.

 Kukonda: Mtu mwenye vidonda vya tumbo hukosa hamu ya kula chakula na hukonda.

Dalili za ugonjwa huu  huweza kuwa mbaya zaidi kama vile kutapika damu, kutoa haja kubwa yenye rangi nyeusi au iliyochanganyikana na damu nyeusi na kusikia kichefuchefu.

 

 Tiba Ya Vidonda Vya Tumbo

 

Tiba ya vidonda vya tumbo hutolewa kulingana na chanzo kilichosababisha ugonjwa huo kama ni bacteria au matumizi ya dawa. Lengo kubwa ni kupunguza makali ya tindikali katika tumbo ili vidonda vipone au kuua bacteria wanaosababisha ugonjwa huu.

 1. Dawa za Kuua bacteria (antibiotics) wa H. pyroli

Kama daktari atagundua kuwepo wa bacteria wa aina aina ya H. pyroli katika mfumo wako wa uyeyushaji chakula, atakuandikia mchanganyiko wa dawa za kuua bacteria hao ambazo utazitumia kwa kipindi cha angalau wiki mbili pamoja na dawa nyingine za kupunguza tindikali katika tumbo.

 2. Dawa za kuzuia utengenezaji wa tindikali na kusaidia uponyaji

Dawa hizi ambazo huitwa Proton Pump Inhibitors (PPIs) hupunguza tindikali katika tumbo kwa kuzuia ufanyaji kazi wa seli zinazohusika katika kutengeneza tindikali. Dawa hizi ni kama omeprazole (Prilosec), lansoprazole (Prevacid), rabeprazole (Aciphex), esomeprazole (Nexium) na pantoprazole (Protonix).

3. Dawa za kupunguza utengenezaji wa tindikali

Dawa hizi huitwa acid blockers au histamine (H-2) blockers. Hizi ni dawa zinazofanya kazi kwa kupunguza kiwango cha tindikali itakayoingizwa kwenye mfumo wa uyeyushaji chakula hivyo kupunguza maumivu na kusaidia uponyaji. Mfano wa dawa hizi ni ranitidine (Zantac), famotidine (Pepcid), cimetidine (Tagamet) na nizatidine (Axid).

 4. Matumizi ya antacids kupunguza makali ya tindikali

Dawa hizi hupunguza makali ya tindikali ambayo tayari ipo ndani ya tumbo na kumpa mgonjwa nafuu ya mara moja. Dawa hizi si za kuponya ugonjwa huu bali kukupa nafuu ya muda mfupi tu.

 5. Dawa za kulinda kuta za mfuko wa tumbo na utumbo mwembamba

Wakati mwingine daktari anaweza kukupa dawa za kulinda kuta za tumbo lako na utumbo mwembamba. Dawa hizi huitwa cytoprotective agents, nazo ni kama sucralfate (Carafate), misoprostol (Cytotec) na bismuth subsalicylate (Pepto-Bismol).

 

Mada yetu ya leo imeeleza maana ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo na vyanzo vya ugonjwa huo. Tukazungumzia dalili za kuweza kutambua kama unaumwa vidonda vya tumbo. Na mwisho tukaoorodhesha dawa za vidonda vya tumbo. Matumaini yetu ni kwamba umejifunza na kuuelewa ugonjwa huu. Katika mada yetu ijayo tutazungumzia ugonjwa wa stroke na kuona unasababishwa na nini. Usikose kuwa nasi.

Tunaomba usisite kutoa maoni yako kuhusu uandishi wa mada hii au kutoa maswali uliyo nayo. Ni furaha yetu kuona kwamba tumekujibu vizuri pale ulipokuwa na swali.

Kama una tatizo la ugonjwa huu na bado hujapata tiba kamili, tuandikie au tupigie simu kwa anuani zifuatazo:

promota927@gmail.com, simu 0655 858027 na 0756 181651 au jaza fomu utakayoiona chini kwenye ukurasa huu.

 

Jina Lako

Anuani Ya Barua Pepe

Namba Yako Ya Simu

Kichwa Cha Habari

Swali Au Maoni Yako

Pata Mahitaji Yako Ya Dawa Za Nje Kwa Matatizo Yanayokusumbua Ukiwa Tanzania. Boresha Afya Yako Kupitia Tovuti Hii

404 Not Found

404 Not Found


nginx/1.10.3