Mwanamke anayeshindwa kupata mtoto huitwa kwa majina mengi katika lugha yetu. Majina kama mgumba au tasa ni majina
yaliyozoeleka. Tatizo hili huathiri mamilioni ya familia na inakadiriwa kuwa asilimia 10 hadi 15 ya familia hupata tatizo la mwanamke kutopata ujauzito au kutozaa mtoto hai. Katika ukurasa huu tutaona sababu za mwanamke kukosa mtoto au sababu za mwanamke kukosa kizazi na kujadili hatua ambazo wanandoa wanaweza kuzichukua kuondokana na tatizo hilo.
Tatizo la mwanake kushindwa kupata ujauzito halitokani na mwanamke pekee, yawezekana kuwa mwanamke ndiye mgumba
(tasa) au mwanamme ndiye chanzo cha tatizo. Wakati mwingine wote wawili huwa wana matatizo. Inakadiriwa kuwa matatizo ya wanawake yanachangia theluthi moja ya ndoa zinazokosa watoto, ya wanaume yanachangia pia theluthi moja na theluthi inayobakia huchangiwa na sababu ambazo au hazijulikani au ambazo zinazotokana na mchanganyiko wa matatizo ya jinsia zote mbili.
Ugumba au utasa maana yake ni kuwa mwanamke ameshindwa kupata ujauzito baada ya mwanamme na mwanamke kujamiiana
kikawaida bila kinga katika kipindi cha mwaka mmoja au katika kipindi cha miezi 6 kama mwanamke ana umri wa zaidi ya miaka 35. Tafsiri hii pia hutumika kwa wanawake wanaoshindwa kutunza mimba hadi kuzaa kiumbe hai. Kuna aina mbili za ugumba. Primary infertlity ni tatizo la kutopata mtoto kwa wawili ambao wote hawajawahi kupata mtoto kabla na secondary infertility ni tatizo la kutopata ujauzito kwa wawili ambao kati yao mmoja au wote wawili walishawahi kupata mtoto kabla.
Ni jambo gumu kidogo kutambua sababu za ugumba kwa mwanamke lakini kuna aina nyingi za tiba kwa tatizo hili. Aina
ya tiba atakayopewa mwanamke itaendana na aina ya tatizo alilo nalo. Si mara zote mwanamke atahitaji kupata tiba – wanafamilia wengi wamekuja kupata watoto wenyewe bila tiba yo yote.
Ugumba Wa Mwanamme
Kwa sababu tumeona hapo juu kuwa mwanamme na mwanamke wanachangia tatizo la kukosa mimba kwa viwango sawa, hatuna
budi kulitazama tatizo hili la ugumba kwa mwanamme. Ni imani iliyotawala hapo zamani kuwa endapo mwanamke hakupata mimba, basi mwanamke huyo ndiye aliyekuwa na tatizo. Ni vizuri kwa hiyo wote wawili mwanamke na mwanamme kuchukuliwa vipimo ili kujua ni nani baina yao ndiye mwenye tatizo.
Ugumba wa mwanamme ni mwanamme kushindwa kumpa ujauzito mwanamke baada ya kujamiiana na mwanamke bila kinga katika
kipindi cha mwaka mmoja.
Matatizo ya ugumba kwa mwanamme karibu yote yanahusiana na shahawa (manii) – uwingi wa shahawa (sperm count) au ubora wa shahawa (quality of sperm)
Matatizo hayo ni kama yafuatayo:
– Kiwango kidogo cha manii (low sperm count)
– Manii au shahawa zinashoshindwa kutembea haraka – zinazokufa kabla ya kulifikia yai
– Shahawa ambazo zina dosari kimaumbile
– Ute (seminal fluid) uliozidi uzito – shahawa zinashindwa kuogelea ndani yake kirahisi
– Ukosefu wa shahawa
– Kuwa na upungufu au kiwango kilichozidi cha homoni zinazoongoza uzalishaji wa shahawa
Chanzo kingine cha ugumba kwa wanaume kinahusiana na utoaji (umwagaji) wa shahawa. Wakati mwingine mirija katika kiungo cha uzazi cha mwanamme huziba na kusababisha umwagaji wa shahawa wa shida au kutomwaga shahawa kabisa wakati mwamme anapofika kileleni. Kuna wakati shahawa huweza kurudi kutoka kwenye tezi dume (prostate ) hadi kwenye kibofu (bladder) badala ya kutoka nje ya mwili.
Wakati mwingine chanzo cha ugumba kwa mwanamme hakieleweki kabisa. Huu ni ugumba usioeleweka (unexplained infertility). Hata kama mwanamme anabainika na ugumba huu usioeleweka, bado kuna tiba za kujaribu.
Sababu Za Ugumba Kwa Mwanamme
Kuna vitu ambavyo huongeza uwezekano wa mwanamme kupatwa na tatizo la kushindwa kumpa mwanamke mimba. Baadhi ya
sababu ni kama zifuatazo:
– Tiba za chemotherapy au za kutumia mionzi
– Sumu kwenye mazingira, kama madini ya lead na dawa za kuulia wadudu
– Kutumia pombe kupita kiasi
– Kuumia sehemu za mfuko wa pumbu au pumbu zenyewe
– Uvutaji wa sigara
– Pumbu kupata joto kupita kiasi kutokana na kuvaa nguo zinazobana sana, kuogelea katika au kuoga maji ya moto
– Kuwa na pumbu ambazo hazijatoka na kuning’inia nje ya mwili
– Varicocele – Kuvimba kwa mishipa ya damu ya veni inayozunguka mfuko wa korodani
Tiba Ya Ugumba Kwa Mwanamme
Tiba kwa mwanamme anayeshindwa kumpa mwanamke mimba hutolewa kulingana na aina ya tatizo alilo nalo. Baadhi ya njia
zinazotumika ni kama ifuatavyo:
1. Upasuaji: Upasuaji hufanywa kurekebisha matatizo ya kimaumbile au uharibifu uliotokea kwenye viungo vya uzazi.
Upasuaji pia hufanywa kurekebisha mirija ya kusafirisha shahawa iliyoziba na kuripea mishipa ya veni iliyovimba (varicocele) inayozunguka mfuko wa korodani.
2. Dawa, vitamini na virutubishi: Vitu hivi hutumika kuondoa vyanzo vya ugumba kama matatizo ya homoni (hormone
imbalances) na jogoo kushindwa kuwika.
3. Intrauterine insemination (IUI) – shahawa za mwanamme huchukuliwa na huchujwa kiutaalamu “sperm washing”
kutenganisha shahawa safi na dhaifu. Mhudumu wa afya huweka shahawa safi kwenye nyumba ya uzazi ya mwanamke (uterus) hivyo kupunguza umbali kati ya mbegu za kiume na yai. Hii pia huitwa donor insemination, alternative insemination, au artificial insemination.
4. In vitro fertilization (IVF) – Mwanamke hupewa dawa ili kuwivisha mayai kadhaa kwa wakati mmoja. Mbegu kutoka kwa
mwanamme huchanganywa na mayai hayo kwenye maabara. Baada ya mayai kadhaa kupevushwa, moja au zaidi ya moja huwekwa
kwenye nyumba ya uzazi ya mwanamke (uterus).
Katika mfululizo wa mada hii, tumejadili maana ya mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kuona awamu nne za mzunguko wa hedhi kwa mwanamke. Tumeona pia sababu za ugumba kwa mwanamme. Tumejadili kwa kina sababu za mwanamke kukosa mtoto na kuelezea tiba za ugumba kwa mwanamke.
Baada ya kulitazama tatizo la ugumba kwa mwanamme, tutalijadili tatizo hili kwa upande wa wanawake katika ukurasa unaofuata “Sababu Za Ugumba Kwa Mwanamke Na Jinsi ya Kuutibu“.
Usisite kuuliza maswali au kutoa machango wako wa mawazo kuhuisana na mada hii. Tutafurahi kukujibu na kupokea mchango wako.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.