Mada yetu ya leo itazungumzia tatizo linalowapata watu wengi , wake kwa waume, kwenye sehemu zao za kutolea haja kubwa. Iwapo utapata maumivu kwenye eneo la haja kubwa, ukiona damu au pengine utaona vijinyama vinaning’inia, yaweza kuwa tayari ni mhanga wa tatizo tunalolichambua hivi leo. Mara nyingi dalili hizi hazileti usumbufu mkubwa na huondoka zenyewe bila tiba. Endapo tiba itahitajika, huweza kutolewa na kulimaliza tatizo. Kwa kiswahili, tatizo hili huitwa bawasiri.
Bawasiri ni uvimbe unaoota ndani na/au kuzunguka tundu la kutolea haja kubwa.
Awali ya yote, tutaona bawasiri ni nini, kisha tutajadili aina zake, sababu ya uwepo wake na mwisho kabisa, tiba ambazo zinaweza kutolewa kuondoa tatizo hilo.
Sehemu ya mwisho ya utumbo mkubwa iitwayo anal canal ina urefu wa kiasi cha sentimeta 4 hivi. Sehemu ya chini kabisa ya anal canal ni tundu la kutolea kinyesi nje ya mwili (mkundu). Sehemu ya juu yake inaungana na rectum ambayo pia ni sehemu ya utumbo mpana.
Kuna mtandao wa veni ndogo (mishipa ya damu) kwenye ngozi inayofunika anal canal. Mara nyingine veni hizi hupanuka na kuruhusu damu nyingi na kuzifanya zitune. Veni hizi zilizotuna na tishu zinazozizunguka zinaweza kutegeneza uvimbe kwenye eneo moja au zaidi, na hii ndiyo huitwa bawasiri, kwa kiingereza piles au pathological hemorrhoids.
Kuna Aina Ngapi Za Bawasiri?
Bawasiri za ndani (Internal piles ) ni zile zinazotokea kwenye eneo la ndani lililo zaidi ya sentimenta 2-3 kutoka kwenye tundu la kutolea kinyesi – kwenye eneo la juu la anal canal. Bawasiri za ndani kwa kawaida hazina maumivu kwa sababu sehemu ya juu ya anal canal haina nyuzi za neva za maumivu.
Bawasiri za nje (Exteranl piles) ni zile zinazotokea kwenye eneo lililo chini yake, eneo la chini la anal canal. Bawasiri za nje zaweza kuwa na maumivu kwa sababu eneo la chini la anal canal lina uwingi wa nyuzi za neva za maumivu.
Watu wengine huwa na bawasiri za ndani na bawasiri za nje kwa wakati mmoja.
Bawasiri za ndani hupangwa kwa grade, grade 1 hadi 4 kulingana na madhara na ukubwa wake:
Grade 1: Ni uvimbe mdogo kwenye ngozi inayotanda anal canal kwa ndani. Ni uvimbe ambao hauonekani au huwezi kuugusa kutokea nje. Bawasiri za aina hii huwapata watu wengi. Bawasiri hizi huweza kukua na kuingia kundi la pili – Grade 2.
Grade 2: Bawasiri hizi ni kubwa zaidi. Huweza kujitokeza na kuchungulia nje ya tundu la haja kubwa wakati ukijisaidia lakini hurudi ndani mara moja baadaye.
Grade 3: Ni bawasiri zinazoning’inia nje ya tundu la haja kubwa wakati ukielekea msalani. Unaweza kuvisikia kama vinjinyama kimoja au zaidi vinavyoning’inia nje ya tundu. Ni vijinyama ambavyo unaweza kuvisukumizia ndani kwa kidole.
Grade 4: Ni vijinyama ambavyo huning’inia wakati wote nje ya tundu la haja kubwa na huwezi kuvisukumizia kwa ndani kwa kidole. Mara nyingine vinaweza kuwa vibonge vikubwa vya nyama.
Bawasiri Husababishwa Na Nini?
Sababu kamili inayofanya mabadiliko madogo yatokee kwenye veni zilizoko kwenye utando unaofunika anal canal na kusababisha bawasiri kutokea haijafahamika. Bawasiri nyingine hutokea bila sababu maalumu. Inafikirika kuwa kuongezeka kwa msukumo wa damu kwenye eneo la ndani na linalozunguka tundu la haja kubwa kunaweza kuwa ndiyo sababu kubwa.
Kuna mazingira yanayochangia uwezekano wa kutokea kwa bawasiri kuwa mkubwa zaidi, nayo ni:
Kufunga Choo: Kutoa kinyesi kikubwa au kujikamua kwa nguvu wakati wa kujisaidia haja kubwa. Hii huongeza msukumo ndani na kuzunguka veni za kwenye tundu la haja kubwa. Hii inaonekana kuwa ni sababu kubwa ya bawasiri kutokea.
Mimba: Ni kawaida kabisa bawasiri kujitokeza wakati wa uja uzito. Hii labda hutokea kutokana na msukumo unaotokea juu ya rectum na anus kwa kutokana na mtoto kulalia juu ya maeneo hayo na kutokana na matokeo yanayotokana na mabadiliko ya homoni wakati wa uja uzito kwenye veni..
Kuzeeka: Tishu zinazozunguka ndani ya mkundu zinaweza kupoteza nguvu zake kadri umri unavyokuwa mkubwa.
Kurithi: Watu wengine wanaweza kurithi udhaifu wa kuta za veni za kwenye eneo la tundu la haja kubwa.
Sababu nyingine zinajumuisha kunyanyua vitu vizito na kikohozi cha muda mrefu (sugu).
Dalili Za Bawasiri
Dalili za bawasiri hutofautiana. Wakati mwingine hakuna dalili zinazojitokeza na mtu anaweza asijue kuwa ana bawasiri.
Dalili ya kawaida kabisa ni kutokwa na damu wakati ukienda kujisaidia haja kubwa. Damu huonekana iliyo mbichi, nyekundu, juu ya toilet tissue, kwenye sahani ya choo au ikiwa imekizunguka kinyesi.
Bawasiri huweza kuchomoza na kuning’inia nje. Mara nyingi unaweza kuzisukuma na vidole zikarudi ndani baada ya kujisaidia. Lakini bawasiri zilizofikia hali mbaya huning’inia moja kwa moja nje na huweza kuzisukuma ndani.
Bawasiri ndogo za ndani kwa kawaida hazina maumivu. Bawasiri kubwa huweza kutoa majimaji, kuwa na maumivu, na kuwasha. Majimaji yatokayo yanaweza kuchubua eneo linalolizunguka tundu la haja kubwa. Unaweza kuwa na hisia za kuwa na haja kubwa au kuwa hujamaliza vizuri haja zako ukiwa unatoka msalani.
Matokea mabaya ya bawasiri zinazoning’inia ni kuwa zinaweza zikajifinyanga na kusababisha damu kushindwa kupita kuelekea kwenye bawasiri hizo, hali ambayo inaweza kuleta maumivu makali sana. Mara chache inaweza ikatokea kuwa damu ikaganda ndani ya bawasiri (thrombosis) hizo, hali ambayo huleta maumivu makali pia.
Tiba Ya Bawasiri
Kukwepa Kufunga Choo Na Kutumia Nguvu Wakati Wa Haja Kubwa
Jaribu kuweka kinyesi kuwa laini na usitumie nguvu wakati wa kujisaidia haja kubwa. Unaweza kufanya yafuatayo:
Tumia nyuzinyuzi kwa wingi kama matunda, mboga za majani, nafaka n.k.
Tumia vinywaji kwa wingi. Watu wazima yafaa kunywa angalau lita 2 kwa siku (glasi 6-8). Utatoa maji mengi kama mkojo lakini mengine yataingia tumboni na kulainisha kinyesi. Vinywaji vya karibu aina zote vinafaa, lakini pombe husababisha mwili kupoteza maji kwa hiyo siyo nzuri sana. Matumizi ya kahawa kwa wingi nayo siyo mazuri.
Nyuzinyuzi Za Kiada. Kama chakula chenye nyuzi nyuzi kwa wingi hakisaidii, unaweza kutumia nyuzinyuzi za kiada kama ispaghula, methylcellulose, bran au sterculia. Unaweza kuvinunua hivi kutoka kwenye maduka ya madawa. Methylcellulose inasaidia pia kulainisha kinyesi na kukifanya kiweze kupita kirahisi.
Acha kutumia dawa za kupunguza maumivu zenye codeine. Kama co-codamol, kwa sababu nuwa ni chanzo cha kufunga choo. Dawa za kawaida kama paracetamol husaidia.
Kujisaidia Inapotakiwa. Nenda chooni mara moja baada ya kusikia haja kubwa. Watu wengine hujibana na kufikiria kwenda kujisaidia baadaye. Tabia hii hufanya ukubwa na ugumu wa kinyesi kuongezeka na kuleta shida wakati wa kukitoa. Usijikamue kwa nguvu wakati wa haja kubwa. Usitumie muda mwingi chooni, kwani inaweza kusababisha ujikamue. (Kwa mfano, usisome wakati ukiwa chooni).
Hatua hizi zitakusaidia usitokwe na damu au kukosa raha. Inaweza kuwa ni tiba kwa bawasiri ndogo na zisizochomoza na kuning’inia nje (Grade 1). Bawasiri ndogo za garde 1 huweza kuondoka zenyewe baada ya muda.
Mafuta Na Cream
Aina mbalimbali za bidhaa za mafuta na cream zinaweza kutumika. Bidhaa hizi si kwa ajili ya kuponya bawasiri bali kupunguza hali ya kujisikia vibaya na miwasho. Bawasiri za mimba huondoka zenyewe baada ya kujifungua.
Tiba Ya Banding
Banding ni tiba inayotolewa kwa bawasiri za grade 2 au 3. Inaweza pia kutumika kutibu bawasiri za grade 1 pale ambapo hatua za hapo juu zitakuwa hazikusaidia.
Daktari wa upasuaji hutumia vifaa maalumu kuzivuta bawasiri na kufunga rubber band kwenye shina la bawasiri hizo. Kwa kufanya hivyo, damu haitafika kwenye bawasiri hizo, ambapo zitakufa baada ya siku chache. Kidonda hupona chenyewe na kuacha kovu.
Banding ya bawasiri za ndani mara nyingi haileti maumivu kwa sababu vishina vya bawasiri hizo huota kwenye eneo ambalo halina mishipa ya neva. Bawasiri hadi tatu huweza kutibiwa kwa njia hii kwa wakati mmoja.
Asilimia 20 ya bawasiri zilizotibiwa kwa njia hii huweza kuota upya siku za baadaye. Lakini tiba ya banding huweza kurudiwa tena. Uwezekano wa bawasiri kukurudia utakuwa mdogo kama tahadhari zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuacha kujikamua wakati wa haja kubwa.
Watu wachache huweza kupata madhara zaidi baada ya tiba hii, kama kutokwa na damu, matatizo ya kukojoa, maambukizi ya wadudu au kuota uvimbe kwenye eneo lililokuwa na bawasiri.
Tiba Nyingine
Katika kurasa nyingine tumejadili ugonjwa wa homa ya ini (hepatitis) na ugonjwa wa kaswende (syphilis).
Ndugu msomaji, uwe huru kuuliza maswali au kutoa maoni yako kuhusu mada yetu ya leo. Tunaahidi kukujibu kwa wakati mwafaka.
Kwa mawasiliano tuma ujumbe wako kupitia ukurasa huu kwa kujaza fomu hapa chini , au tuma barua pepe kwa anuani promota927@gmail.com au piga simu kwenye nambari zifuatazo: 0655 858027 au 0756 181651.
Tafadhali ungana nasi kwenye ukurasa wa facebook wa LINDA AFYA YAKO ili upate mfululizo wa mada zetu zinazohusu afya ya binadamu na jinsi ya kuanza na kufanya biashara za mtandao zinazohusu virutubisho vya mwili kwa mtaji mdogo kabisa. Tunaomba uweke LIKE kwenye ukurasa huo endapo utakuwa umependezewa na mada zetu.