Gout ni ugonjwa ambao umefahamika kwa miaka mingi sana. Inasadikika kuwa watu wa kwanza kuutambua ugonjwa huu walikuwa watu wa Misri, kunako miaka ya 2640BC. Mtaalamu wao wa tiba Hippocrates aliuita ugonjwa huu “Ugonjwa Wa Kumfanya Mtu Asitembee” na aliuhusisha ugonjwa huu na namna ya mtu anavyoishi. Hadi hivi leo ugonjwa huu ni tatizo la jamii nyingi, ambao huwapa maumivu makali sana wale ambao wameathirika. Kwa bahati nzuri ugonjwa huu hutibika na kuna hatua za kuchukua zinazoeleweka ili usipatwe na ugonjwa huu. Katika ukurasa huu tutatazama ugonjwa wa gout ni nini , chanzo cha ugonjwa wa gout, dalili zake na namna ya kuutibu pale unapokuwa umeathirika.
Gout Ni Nini?
Gout ni namna moja ya Arthritis, ugonjwa ambao hushambulia joints (sehemu za maungio ya mifupa). Huu ndio ugonjwa wa joints ambao huwashambulia sana na kuwapa maumivu makali wanaume. Wanawake pia huweza kuathirika na ugonjwa huu hasa baada ya kukoma hedhi. Ugonjwa huu huleta maumivu makali ya ghafla, hasa kwenye sehemu linapoanzia dole gumba la mguu. Dalili za ugonjwa huanza kuonekana pale uric acid, tindikali ambayo huzalishwa na mwili katika ufanyaji kazi wake (ambayo haina manufaa kwa mwili) inapobakia katika viungo vya mwili na katika majimaji ya mwili. Uric acid iliyoganda (tophi) huweza kujikusanya na kubaki chini ya ngozi inayozunguka joints, huweza pia kujikusanya ndani ya figo na kusababisha kidney stones (namna ya kokoto ndogo ndani ya figo).
Gout inaweza kusababisha madhara ya kudumu kwenye maungio ya mifupa na figo. Endapo hatua za kuutibu ugonjwa huu hazitachukuliwa kwa muda mrefu (miaka 10 au zaidi), madhara ya kudumu humtokea mgonjwa.
Chanzo Cha Gout Ni Nini?
Gout kutokea kimsingi pale tindikali aina ya uric (uric acid) inapozidi kiwango katika mwili wa binadamu hali ambayo kiutaalamu huitwa hyperuricemia. Tindikali hii ni matokeo ya kuvunjwavunjwa na mwili kwa aina fulani za chakula kama nyama, nyama ya kuku na chakula cha baharini. Tindikali hii kwa kawaida huchanganyika na damu na mwisho hutolewa nje ya mwili pamoja na mkojo kupitia figo. Tindikali hii ikitengenezwa kwa wingi mno au isipotolewa nje ya mwili kwa kiwango kinachosatahili, ile inayobakia huganda na kukaa kwenye maeneo ya joints na kusababisha maumivu kwenye joints hizo na maeneo yaliyo karibu. Kuna mazingira ambayo hupelekea hali hii ya uzidifu wa tindikali ya uric katika mwili na mwishowe gout kutokea nayo ni:
- Jinsia: Wanaume huzalisha tindikali ya uric kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko wanawake, viwango vya uzalishaji kwa wanawake vikikaribia vile vya wanaume pale tu wanapokoma hedhi.
- Urithi: Kuzaliwa kwenye familia yenye historia ya gout kunakufanya uwe kwenye hatari kubwa zaidi ya kuupata ugonjwa huu.
- Mtindo wa maisha: Unywaji wa pombe huzuia utolewaji wa uric acid nje ya mwili na ulaji wa chakula chenye purine kwa wingi husababisha kiwango cha tindikali ya uric kuwa kikubwa mwilini.
- Madini ya lead: Kuwa karibu na madini haya kwa muda mrefu kumeonyesha kuhusika na aina fulani za gout.
- Madawa: Baadhi a madawa yameonekana kuongeza kiwango cha uric acid mwilini.
- Unene: Unene umedhihirika kuongeza hatari ya kupatwa na gout.
- Matatizo ya kiafya: Kama figo hazifanyi kazi vizuri kiwango cha uric acid mwilini kitapanda. Matatizo mengine ya kiafya yanayochangia ni high blood pressure (hypertension), kisukari na hypothyroidism.
Dalili Za Gout
Ugonjwa wa gout huanza ghafla na mara nyingi katikati ya usiku. Ugonjwa huanza kwa kuleta maumivu makali kwenye maungio ya mifupa na mara nyingine kuambatana na uvimbe. Gout mara nyingi hushambulia maungio makubwa ya dole gumba la mguu lakini pia huweza kushambulia maungio ya mikono, ankles, viwiko vya mikono na vidole.
Tiba Ya Gout
Matatizo yaliyo mengi ya gout huondolewa kwa kutumia dawa. Nonsteroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs), colchicine au corticosteroids hutumika kuondoa maumivu kwenye eneo lililoathirika na gout.
Dawa nyingine hutumiwa ili kupunguza uzalishaji wa uric acid (xanthine oxidase inhibitors), mfano allopurinol au kuzisaidia figo ziweze kuondoa tindikali ya uric kutoka katika mwili (probenecid).
Mtindo wa maisha unaweza kusaidia katika kupunguza makali ya ugonjwa huu au kuzuia usikupate. Yafaa kufanya yafuatayo:
– Kunywa maji mengi, lita 2-4 kwa siku
– Kutokunywa pombe
– Kuweka uzito wa mwili kwenye kiwango kinachofaa
– Kupata mlo uliokamilika (balanced diet)
– Kutotumia vyakula vyenye purines kwa wingi (vinavyozalisha uric acid kwa wingi). Vyakula vya kukwepa ni kama figo za ng’ombe, maharage na njegele zilizokaushwa, nyama pori, uyoga na maini.
Katika mada ya leo tumeujadili ugonjwa wa gout ambao ni aina moja ya magonjwa ya kundi la Arthritis. Kuweza kuyajua magonjwa mengine ya arthrits usikose kusoma ukurasa wa “Ugonjwa Wa Joints-Arthritis” na ili kujua magonjwa ya mifupa ya mwili wa binadamu rejea ukurasa wetu wa “Maumivu Ya Mifupa“. Tunaomba maoni yako kuhusu uandishi wa mada hii na usisite kuuliza kama una swali lo lote. Furaha yetu ni kuona tumekujibu kiufasaha.
Unaumwa ugonjwa huu wa gout na unahitaji usaidiwe?
Wasiliana nasi kwa kujaza fomu hii hapa chini au tuandikie kupitia promota927@gmail.com. Unaweza pia kuwasiliana nasi kwa simu moja kwa moja kwa nambari 0655 85027 au 0756 181651.